By Calson Mugodo
Ewe Mola mraufu, mie mja wako
mwenye mapungufu nina tamanio na ombi mtimani, ninaomba kwa taadhima nirejeshwe
jadi walipo mababu zangu.
Naam, zamani kusiko na runinga
wala rununu, nisifahamu jambo kuhusu kipakatalishi wala kiotomotela. Huko jadi
sitahitaji senti ili kuyakidhi mahitaji yangu. Iwapo itanipasa nife ili nirejee
jadi, basi nipo radhi kufa, Yarabi, mtume Israili mtoa roho aniburure waama
anibebe hobelahobela hadi kule.
Natamani kukutana naye babu ya babu
yangu, nisiyemfahamu hata jina, nikiulizwa kisa na sababu eti nilikuwa
nikihangaika na madaftari shuleni nisipate muda wa kusikiliza hadithi kutoka
kwa babu kumhusu babu yake. Ninataka kustarehe kwenye kifua kipana cha babu ya
babu yangu, kilichojaa vinyweleo huku
nikiusikiliza taratibu wimbo wa utamaduni unaomtoka kinywani, huku mjomba aliye
stadi wa kupiga ngoma, siku hizi twamuita sogora akitekeleza wajibu wake.
Nataka kwenda jadi ambako ndwele
kama vile kansa na UKIMWI ni visa vya kufikirika. Angecheka sana babu iwapo
ningemweleza kuwa binadamu anaweza kudhoofika akakonda na kukondeana kiasi cha
mbavu zake kuhesabika ubavu baada ya mwingine kutokana na makali ya UKIMWI. Na
iwapo maradhi kama haya yangetokea, hofu haingekuwepo kwani penye wazee
hapaharibiki jambo, wazee wenye hekima wangekusanyika usiku wa manane ama
alfajiri ya majimbi ili kujadili suluhu mwafaka, kisha wangejitoma mwituni au
pangoni na kumtoa kafara beberu kwa mizimu kwa ajili ya taambiko. Kisha wangefanya
wanavyojua wao mpaka mizimu iwaelekeze palipo majani au mizizi iliyo tiba kwa
ugonjwa huo.
Kule jadi swala la ndoa lilikuwa
muswaki. Wanapobalehe maghulamu, wangeelekezwa moja kwa moja hadi jandoni,
kisha ngariba angeruhusiwa kuutekeleza wajibu wake. Kisha wangesalia kule kwa
muda wa takribani miezi sita bila kurejea nyumbani. Wangefundishwa majukumu ya
mwanamume na jinsi ya kuishi na wake zao vile vile namna ya kujitegemea na
kutafuta riziki kwa kuwinda wanyama pori na kupitia zaraa. Kijiji kizima
kingetumbuizwa kwa nyiso zinazoimbwa kila usiku na mashujaa hao walio jandani. Mwana
wa mtu anapotoka jandoni akiwa kwenye pita pita zake, kwenye baraste angekutana
na mwanamwali mrembo kutoka utosini hadi kwenye vidole vya mguu , ghulamu aliyekomaa
tayari kuuasi ukapera angemtamani nusra mate yamdondoke . La kufurahisha ni
kwamba mwanamume huyu asingejisumbua kumshawishi binti huyu aliyefunzwa
unyagoni akaelewa somo, badala yake angehitaji tu kuzungumza na abu yake, kisha
washenga wangetafutwa kupeleka posa kwa wazazi wa binti. Kisha kungefuatia
harusi ya kiasili baada ya mahari kulipwa , kisha wazee wangebugia mvinyo
maalum kama ishara ya makubaliano na ushirikiano. Tena takriban mabinti wote
walikuwa mabikira hadi wakati wa ndoa, ni raha iliyoje? Huko ndiko ninakotaka
kwenda.
Natamani kuwa pamoja na wazee
wangu kando ya miale ya moto, tena moto uliowashwa kwa kuzungusha kipande cha
mti juu ya gogo hadi moto ukatoka bila kutumia kiberiti. Kisha babu angechukua
hatamu na kutamba hadithi zenye mashiko moja baada ya nyingine mpaka mtima
uridhike na kusema tosha. Baadaye tungejikunyata ndani ya jamvi
lililotengenezwa kwa ngozi ya ng'ombe ili angalau tupate usingizi.
Iwapo kungetokea mwizi usiku huo,
akanyatia nyatunyatu na kumchukua ng'ombe mmoja, Babu angeiamkia mizimu na
kufanya anavyojua yeye mpaka yule mwizi amrejeshee ng'ombe na kuomba msamaha.
Kisha babu angemsamehe kwani anafahamu fika ubaya hauondolewi kwa ubaya ila
wema, kwa hivyo, angempa ushauri na maelezo kindakindaki ya jinsi ya
kujitafutia mali yake mwenyewe.
Nikiwa kule sitavitamani vyakula vya
huku kwenu kama vile sharubati na vibanzi , badala yake nitaridhika na kutafuna
minofu ya nyama iliyochomwa na kufukizwa kwa moshi pamoja na vyakula vya kiasili
ikiwemo mizizi na majani ya mimea ainati yenye uwezo wa kukabiliana na magonjwa
yote. Nakomea hapo kwa sasa nitaiendeleza hadithi hino nikirejea kutoka jadi.
No comments:
Post a Comment