ONLINE

Thursday 18 March 2021

Sina chakula wenzangu

  SINA CHAKULA WENZANGU

Na Hosea Namachanja

Kukonda kwangu kukonda, wenzangu ni kuumia,

Maisha yananiponda, hadi siwezi kwongea,

Kila siku ninashinda, mtimani nikilia,

Hino njaa hino njaa, wenzangu yanimaliza,

Asubuhi na jioni, kula kwangu kwa taabu,

Ila wazi kuwambeni, ninaona ni aibu,

Wapo nikiwambieni, watanicheka ajabu,

Hino njaa hino njaa, wenzangu yani,

Midomo mkiniona, wenzangu imekauka,

Huku pia nikinena, kinywani mwangu mwanuka,

Kisa hakika mchana, hakuna kitu mefyeka,

Hino njaa hino njaa, wenzangu yanimaliza,

Nimejawa na madeni, Fuliza na Mshwari,

Nao wazazi nyumbani, menyamaza siyo siri,

Simu kunipigieni, hawapigi siyo siri,

Hino njaa hino njaa, wenzangu yanimaliza,

Ukweli rivasi koli, kwa muda nimejaribu,

Lakini ninasaili, mwanao hawanijibu,

Kwani mimi ni katili, au kipi cha ghadhabu? 

Hino njaa hino njaa, wenzangu yanimaliza,

Mimulodi nimekuwa, kwa sasa mtandaoni,

Mimu ninazipakuwa, kuficha yalo moyoni,

Na tena kutambuliwa, nina shida maishani,

Hino njaa hino njaa, wenzangu yanimaliza,

Wenzangu nimwombe nani, pesa anisaidie?

Wenzangu nimwombe nani, chakula aniitie?

Wenzangu nimwombe nani, chajio nikimbilie?

Hino njaa hino njaa, wenzangu yanimaliza,

Msione nikicheka, mkadhani niko poa,

Kwa ndani ninachomeka, na masaibu hasaa,

Japo kweli kutamka, nashindwa kuwelezea,

Hino njaa hino njaa, wenzangu yanimaliza,

Sijui nilikosani, mimi kweli maishani,

Ndiposa kule nyumbani, sisaidiwi jameni,

Laiti ngalijuweni, nijue la kufanyeni,

Hino njaa hino njaa, wenzangu yanimaliza,

Wiki jana nimewaza, kifo kikanichukue,

Niishie kwenye giza, masomo nijiachie,

Kuliko kujiumiza, mautini nitulie,

Hino njaa hino njaa, wenzangu yanimaliza,

Anisamehe Manani, kwa yale nimewazia,

Machozi anifuteni, kuishe kwangu kulia,

Na mwokozi nipateni, aje na kuniokoa,

Hino njaa hino njaa, wenzangu yanimaliza,

Tamati nikifikia, kwa sasa sina namna,

Waifai najendea, kukaa kule nanena,

Angaa kufikiria, mengi niache wasena,

Hino njaa hino njaa, wenzangu yanimaliza,

No comments:

Post a Comment