ONLINE

Thursday 18 March 2021

Kitumbua kimeingia mchanga

 MSUMARI MOTO: MBONA NDOA NYINGI KARNE HII HAZIDUMU?


"Ni dunia hubadilika au watu ndio hubadilika? " Aliniuliza mzee mmoja mwaka uliopita na kuongeza kuwa nisimjibu jibu nililokuwa nalo ila nijiwekee mwenyewe. Hata hivyo, alinisimulia machache yanayohusu uchumba enzi zake za ujana ambayo baadhi yayo, mwenyewe nimeyashuhudia katika maisha yangu.


Kale, palikuwapo kitanda cha mikanda ambacho kilipewa jina "kitanda cha spring'i". Jina hilo lilitokana na tabia zake wakati mtu amekilalia. Kuchao, kilikuwa cha kumchezesha mtu huku na kule namna spring'i za vyombo vya usafiri zilivyo.


Kwa hivyo, katika ndoa, wanandoa walikipenda sana kitanda hicho kwa sababu, hamna mume au mke angelala na mchumba wake bila kutatua mzozo wa uchumba uliozuka. Hata kama mmoja angekuwa na hasira nyingi, usiku kitanda kile kingetingika na kumsukuma hadi alipo mpenziwe wakati wa kujinyosha.


Ikilinganishwa na leo, mabahari ya vitanda vyumbani hayasaidii chochote. Mtu atapinda mgongo kule na mwingine kule na walale bila kuutatua mzozo wa ndoani. Fauka ya hili, ndoa nyingi katika karne hii yetu zasambaratika kwa sababu zifuatazo:


Kutoaminiana. Wengi wa wanandoa wameyafanya mapenzi kama kazi ya kibarua ambapo, baada ya kazi, mtu analipwa na kuenda zake. Hayaheshimiwi katu. Wengi wanaoana bila mpango au msimamo wa maisha au kuwa tayari kuwa katika ndoa ndiposa kila uchao, wengi huchepuka watakavyo kani ya kuwapata watoto nje ya ndoa.


Shinikizo la wanarika. Suala hili ni hatari sana kuliko kiharusi. Wengi wa vijana wa leo huingia kwenye ndoa kwa sababu "fulani" kaoa au kaolewa na "yeye" bado kuulizwa ulizwa na wenzake idadi ya watoto alio nao, mahali huishi na mkewe au mumewe na maendeleo ya familia "nyumbani." Hili huwafanya kukimbilia ndoa bila maono.


Unafiki wakati wa kuchumbiana. Inafaa wakati wa kuchumbiana, wachumba tarajiwa kuyaweka mambo yao wazi ili kila mmoja ajue hali ya maisha ya mwingine. Wengi wao wakati wa kuchumbia huwa wajanja kwa kujiinua huku wakiwa hawana kitu ila uongo mtupu. Jambo hili hushusha hadhi ya imani ya uaminivu katika ndoa na pia hata kuvunjika hasa ikibainika mmoja ni mraibu wa mihadarati huku mwingine ni wa injili ya mbinguni.


Kutowajibika katika ndoa. Inasikitisha sana katika jamii ya leo kupata watoto wadogo wakichuuza sokoni kisa na maana wazazi wao waliwatwika hilo jukumu. Jambo hili ni ishara tosha kwamba, baba mzazi wa mtoto huyo hawajibiki katika malezi ya familia (iwapo yu hai) au kinyume kwa mama mzazi. Umaskini katika ndoa hutokana na kutowajibika jambo ambalo wanaume wengi siku hizi huachwa kwa mataa kisa "hawajui kuhangaikia familia."


Tamaa ya mali. Ole wao wanandoa wa usasaleo kwa kukimbilia mali! Awe amesoma au hajasoma, msichana wa sasa hashikiki katika uteuzi wa mchumba sawa na baadhi ya waume wanaoangalia maumbile badala ya vitu vingine pia. Mabinti wengi waolewa kama "mpango wa kando" kwa kuvutiwa na pesa, kazi au sifa alizonazo mwanaume. Hawajali awatongozaye ameoa au hajaoa. Lao ni pesa tu sawa na baadhi ya waume.


Fauka ya sababu hizi miongoni mwa zingine nyingi, ipo haja ya wale ambao hawajaingia au kujisajili katika shule ya ndoa kujifunza kwa wale waliowatangulia katika maisha ya ndoa ambayo huyapitia au waliyapitia ili ndoa zao zidumu kama za wazee wa kale.

      

            Chozi la Kunguni

No comments:

Post a Comment