ONLINE

Monday, 11 July 2016

MASHETANI


Na Amadioha Wa Nzanze


Uongozi na mamlaka ni hadhi ambazo karibu kila mwanadamu humezea mate.Huku kunamaanisha ya kwamba huenda usijue ni nani kiongozi  bora na ni nani kiongozi wa kupanga tu hasa ukizingatia misingi ya miungano ya makabila maarufu kama ‘coalition” iliotawala nchi ya kenya.

Ebrahim Hussein katika tamthilia yake ya MASHETANI, anaonyesha jinsi kuna mtafaruku wa kimatabaka unaeondelezwa hasa na viongozi weusi.Viongozi hawa hawapo tu katika  visiwa vya Zanzibar kama alivyoelezea mtaalam huyu wa fasihi,bali pia hapa chuoni.Ni vigumu kutambua ni kiongozi yupi aliyebora na ni yupi anyetaka tu kula nyama ya mapaja pindi tu anapochaguliwa kutokana na fedha za kuendesha mwili uitwao MUSO kila mwanzo wa mwaka kwenye kalenda ya kiakademia.

Tunapowachagua viongozi kwa misingi ya ukabila,tunakuza na kuendeleza mashetani yatakayotukwaruza,yatufyonze damu yote,yatufifishe na kutufanya kuwa kama ombwe tupu na wenye wingi wa ubwege.utakuwa ni kama msiba wa kujitakia!

Utakapokuwa ukifurahia kupindukia kwa kupitisha mwanasiasa wa kabila lenu,ikumbukwe ya kwamba faida utakazopata  ni finyu au hata huenda usipate faida yoyote kabisa! Huenda shetani autupe uso wako jehanamu utakakosahaulika kwa miaka na mikaka. Isitoshe,watazizonga akili zako kwa mbinu zao za kishetani ukakosa pungwa,wakakufanya uwe shaghalabaghala na mharibifu wa majina hata  kukufanya uwe na utashi wa kuwasafirisha wenzako hadi akhera. Iwapo tu mashetani hayo yatashindwa kwenye chaguzi hizo.

Usishangae kuyapata mashetani yenyewe yakiwa salama wa salmini huku binadamu wakipiga usiahi,wakiugua kwa maumivu ya majeraha ya  vita hivi vya mau mau.La kuatua moyo zaidi ni kwamba,huenda wengine wao watakuwa  katika vicheko vikubwa vya kishetani huku wewe ukiwa katika harakati zako za ugua pole!

Iwapo hatutafanya uteuzi wa moyoni na kukosa kuzuumu kuwachagua viongozi bora na sio bora viongozi,basi maudhui ya tamthilia ya mashetani yataendelezwa leo,kesho na hata milele, sio tu katika chuo hiki cha kifahari bali pia katika nchi yetu kwa uwanda mpana.

Fedha zako,takriban shilingi mia tano kwa mwaka ndiyo damu yako. Damu yenye afya na uzuri wa kupindukia. Damu isiyo na virusi vya aina yoyote.Damu hii itakumbatiwa na kufyonzwa na shetani iwapo hutakuwa mwangalifu.Kwa upande mwingine,iwapo utamchagua kiongozi bora,damu hii itahifadhiwa na kutumika vyema na kistaarabu katika kuunusuru mwili wetu uliyo katika hali mahututi na unaohofiwa na wengi, kufa wakati wowote toka sasa. mwili unaojulikana kwa jina ;MUSO.
Sote tutaamali.

No comments:

Post a Comment