ONLINE

Friday 3 June 2016

MAJI HUFUATA MKONDO





Siasa za Kenya zitasalia kuwa shindano la kikabila.Kauli mbiu imesalia chetu ni chetu....J

Jamii mbalimbali hupigania nyadhifa za uongozi serikalini kama njia ya kunasa njia za uzalishaji asali.Miungano ya kisiasa huundwa kwa misingi ya kikabila na matokeo kuwa wengi wape.Wamezidi kuhubiri amani na utangamano baina ya Wakenya bali mikononi wamebeba panga.Wanakashifu ukabila kwa kampeni mbalimbali wakati wa mchana na usiku kufanya kinyume.Uteuzi katika nyadhifa mbalimbali serikalini kigezo ni kabila ili kupata uungwaji mkono kisiasa kutoka kabila hilo.Mfumo huu umefanya vita dhidi ya ukabila kusalia ruwaza isiyotimika...

Vyuo vikuu nchini vimehalalisha msemo wa maji hufuata mkondo.Wanafunzi hukaa pamoja katika vyumba vya malazi,husoma pamoja na hata kutembea pamoja bali wakati wa uchaguzi hutengana kwa misingi ya kikabila.Huchagua viongozi ili kuwakilisha matakwa ya kabila fulani na kusababisha uongozi duni vyuoni.Hii imetokana na mfano mbaya kutoka kwa viongozi wa kitaifa.Waliotangulia vyuoni pia waliweka misingi hii na vizazi vya baadaye hurithi hulka hizi potovu.

Fujo na vita vya kikabila hutokea mara nyingi baina ya wasomi vyuoni kutokana na siasa.Wanafunzi huwapiga wenzao na kuwajeruhi na hata wengine kuaga dunia kama nduli wasiowajua.Huu ni ukosefu wa utu na ishara ya uchochole wa maadili katika jamii ya wasomi.Walimu,Wanahabari,Wahandisi na Wanasayansi wa baadaye hugeuka na kuwa "Wanajeshi" chini ya Makamanda wanafiki.

Kura baadaye hupigwa na miungano mbalimbali ya kikabila kukidhi matakwa ya nafsi zao.Wao huwa na imani na matarajio kuwa ahadi walizopewa kama jamii katika jamii ya wanazuo zitaafikiwa.Viongozi hawa huwahudumia wanafunzi kutoka jamii zao kwa sababu ni wao waliowawezesha kuzichukua nyadhifa hizo za uongozi,jambo linalozua uhasama wa kikabila.

Hapa Chuoni wanafunzi wana mwelekeo hasi kwa viongozi waliowachagua wao wenyewe.Wamesahau viongozi hawa ni kioo halisi cha waliowapigia kura.Kila mara wanafunzi hulalamikia uongozi mbaya chuoni.Swali wasilojiuliza kuwa chanzo ni nini? Waliowatangulia walishindwa kuziba ufa na itabidi kujenga ukuta.

Ili kuleta uongozi ulio na ufaafu kwa wanazuo hapa chuoni ni muhimu kuvlia njuga mchakato mzima wa kuelimishana kuhusu madhara ya ukabila, wanafunzi wenyewe kuukashifu ukabila.Ndoto ya kuumaliza ukabila itasalia ndoto hadi pale ambapo jamii kwa ujumla itaamua kubadili mienendo na kukosa kufuata mkondo. RJ

No comments:

Post a Comment