Baada ya msururu wa ushindi wa mechi kadhaa bila kusahau kutwaa kombe la Carabao jumapili iliyopita,hatimaye Manchester United wapokea kipigo kilichowaacha wengi vinywa wazi.Hiki ndicho kipigo kikubwa zaidi kunakiliwa msimu huu katika ligi kuu ya Uingereza .Vilevile, ilikuwa historia hasi kunakiliwa kwa upande wa Manchester United katika karne ya ishirini na moja .
Kambi yote ya wababe hawa wa Ulaya ilionekana kutoyaamini
macho yao toka kwa mkufunzi wa hapo
awali , Sir Alex Ferguson hadi mkufunzi wa sasa ,Eric Ten Hag ambaye bado
alikuwa mgeni katika ligi kuu ya Uingereza. Kwingineko, nyuso za mashabiki wa Manchester
united zilisheheni soni na ghadhabu dhihirisho wazi la kutamaushwa na matokeo
hayo.
Upande wa pili, ilikuwa furaha si haba miongoni mwa kikosi
cha Liverpool kwani, kila mshambulizi aliyesajiliwa msimu huu alizitikisa nyavu
mara si moja; sisemi Darwin Nunez bali pia Gakpo . Pamoja nao walikuwa
mashabiki wa timu zenye uhasama na Manchester
united; hii ni ikiwemo Arsenal, Chelsea na Manchester city ambao waliusherehekea
ushindi huo kote nchini sisemi mitandaoni,katika vyumba vinavyouzwa vileo na
hata vyuoni ungedhani timu zao ndizo zilizoshinda.
Timu zote zilionekana kutoshana nguvu dakika arubaini za kwanza.Aidha,ngome ya ulinzi ya Manchester United ilishindwa kustahimili makali ya washambulizi wa Liverpool .Baada ya kulaza damu katika dakika ya arubaini na mbili , Cody Gakpo alitia wavuni bao lililowaweka Liverpool kifua mbele katika kipindi cha kwanza.Hapo awali Marcus Rashford alikuwa keshapata nafasi ya kucheka na wavu ila mlindalango wa Liverpool alionyesha umahiri wake kwa kulinyaka shoti hilo kwa urahisi.
Licha ya Wout Weghorst na Diogo Dalot kuonyesha mchezo wenye
kiwango cha chini,Ten Hag alionekana kuwa na imani nao kipindi cha pili kwani
hakufanya badiliko lolote la kuwatoa mwanzoni mwa kipindi cha pili.
Kipindi cha pili kilipong’oa nanga ,dakika hazikuzidi tatu Liverpool wakaongeza bao la pili kupitia kwa mshambulizi Darwin Nunez .Kila kiungo cha Manchester United wakati huu kilionekana kujisahau kwani dakika ya hamsini Cody Gakpo aliongeza bao lake la pili na kuifanya timu yake kuongeza ushindi wao kwa mabao matatu bila jawabu.
Kadri muda ulivyoyoyoma mbinu za mibabe hii kutoka jiji la
Manchester zilionekana kulemaa na hivyo kumlazimu Mkufunzi wao kufanya mabadiliko
mawili dakika ya hamsini na nane. Hata
baada ya mabadiliko hayo,wapinzani wao walionekana kuwazidi katika safu zote si
ushambulizi tu bali pia viungo.
Kama ilivyo ada yake, Mohammed Salah aliyafichua makucha
yake dakika ya sitini na sita alipofyatua kombora lililomwacha De Gea hohehahe
na hivyo kuongeza idadi ya mabao hadi manne. Wana Liverpool walionekana kutotosheka
na mabao kwani dakika tisa baadaye , Henderson,kiungo
wa Liverpool alimmegea Darwin Nunez krosi ambayo Nunez alitumia kichwa chake
kuiunganisha na kucheka na wavu kwa mara ya pili.
Liverpool walifanya mabadiliko yao dakika ya sabini na nane,
sabini na tisa na themanini na tano mtawalia. Wapinzani wao kwa upande mwingine
walimalizia mabadiliko yaliyosalia dakika ya sabini na saba na themanini na
tano mtawalia.
Mnamo dakika ya themathini na tatu ,Salah alitia kimiani bao
la sita alilolisherehekea kwa kuivua
jezi yake.Tukio hili lilimfanya aadhibiwe kwa kupewa kadi ya manjano.Dakika
mbili kabla ya mechi kutamatika,Roberto Firmino aliyekuwa mchezaji wa akiba
alitamatisha karamu ya mabao kwa kufunga bao la saba.
“Wasio na taaluma.”Ten Hag alithibitisha katika uchambuzi wa
baada ya mechi . Kipindi cha pili kilikuwa dhihirisho wazi wa aliyoyasema Ten Hag.
Kikosi chake kilikosa dira ama kwa uhakika. Walishindwa kuidhibiti kasi ya mchezo kinyume cha wapinzani wao walioonekana kuwa watulivu
licha ya shinikizo kutoka kwa washambulizi kama Marcus Rashford. Baadhi ya
wachezaji walionyooshewa vidole kwa kuchangia ushinde huo ni pamoja na Wout
Weghorst,Diogo Dalot,Luke Shaw na Rafael Varane.
No comments:
Post a Comment