ONLINE

Friday 16 July 2021

Chokoraa


Wavyele walifariki, nilipokuwa mchanga,

Peke yangu nikabaki, na kwanza kutangatanga,

Kuyatafuta mabaki, ya chakula huku Tanga,

Mie kuwa chokoraa, jamii linisahau,


Niligongwa mi na gari, nikienda sikulini,

Hali haikuwa shwari, nikajipata wadini,

Nilipokuwa vizuri, bili haikuwa chini,

Mie kuwa chokoraa, nilachwa sipitalini,


Nilikuwa mi mjinga, mjinga wa darasani,

Nikaenda kwa mganga, niwe mwiba masomoni,

Ila kweli ninalonga, ndipo kushindwa jamani,.

Mie kuwa chokoraa, nilifukuzwa nyumbani,


Kazi nyingi za shokoa, nilifanyiswa nyumbani,

Sikua ninapumua, nikiingia shambani,

Ngejaribu kuongea, ningepigwa si utani,

Mie kuwa chokoraa, chanzo ni mama wa kambo,


Maisha ni mshumaa, usokuwa na mkesha,

Jiji ndo nilikulia, na kuzoea maisha,

Risavu lipohamia, starehe ziliisha,

Mie kuwa chokoraa, risavu hakuna raha,


Laiti ningalijua, singalikula mi karo,

Kwa ujinga nawambia, niliila kweli karo,

Nyumbani sikurejea, baada ya kula karo,

Mie kuwa chokoraa, ujinga wa kula karo,


Kwa upande wangu mie, nilizaliwa mjini,

Msojua na mjue, kakulia humu ndani,

Ya kwangu msishangae, kila kitu mi pipani,

Mie kuwa chokoraa, wazazi machokoraa,


Kila mwana na sababu, ya kuishi mtaani,

Wengi wao masaibu, yalowakumba jamani,

Ni mengi yaliwasibu, wakajipata mijini,

Mie kuwa chokoraa, kaniacha humu mama,


Na Chozi la Kunguni


No comments:

Post a Comment