Na SIMIYU wanyonyi
Nina wingi wa matumaini ya kuwa mtasoma na kuelewa ujumbe huu. Naomba kupewa fursa kusema nanyi, muda mchache tu baada ya kuchaguliwa kwenu kuwa viongozi wa MUSO. Awali ya yote, ningependa kuwapa pongezi. Pongezi kwa juhudi zenu tangu semesta ianze. Mmeyapitia mengi: si milima na mabonde, si raha na karaha, si howe na bezo, si kufumwa kwa maneno ya kuchefua na yale la kuwapa tumaini. Kwa yote hayo, mlistahimili hadi mwisho. Mlipopokezwa medali kwa ushindi, mlishusha pumzi zenu. Matunda ya juhudi zenu yakawa paruwanja. Kigoda sasa, mmekikalia.
Nimechaguwa kuanza nanyi katika msururu huu wa uandishi wa barua kwa kuwa, kando na kushikilia nyadhifa kuu zaidi ndani ya meli ya MUSO, pia nyie ni wagombea mliochaguliwa kwa kura zilizozidi 2000. Kwa kigezo hicho, ni yakini kuwa mliaminiwa zaidi na makomredi. Wanasema, penye uvuli ndipo niwekapo mwanangu. Makomredi waliamini hilo kabla ya kufanya uamuzi wa kuwachagua. Nina maombi kadhaa kweni.
TOWETT NGETICH . Rais wa MUSO. Uaminifu wetu kwako natumai hautatuponza. Meli ya MUSO kabla ukalie kigoda cha Urais, imekuwa katika hali ya kuyumbayumba kiasi kwamba, kosa dogo tu litaizamisha meli. Viongozi wa awali, walikuwa wakitumia meli hii kama chemchemi ya kujaza mafuko yao, kufurisha miili yao ambapo badala ya tumbo, walimiliki viriba. Ahadi kwenye manifesto zao, walizificha zisionekane tena. Badala ya kuwa watetezi wa komredi, walikuwa vijiko vya kuwapakua na kuwaangusha kwenye makaa ya moto wa seneti. Usaliti ati,vibaraka wa utawala mkuu. Walivuja pesa za makomredi kana kwamba wanajilipa madeni waliokopesha makomredi. Meli inayumba. Ndiyo maana, siku hizi humu, sera hazimtoi nyoka pangoni. Humu, ungwana haufai, bora pesa. Kama sivyo basi, kabila lako litakubeba. Idhibati ya haya nisemayo ni jinsi ulivyochaguliwa kutokana na juhudi za makabila ya Kalenjin na Luyha, KALE-LUYHA. Lakini je, utakiuka desturi za watangulizi wako na kuwa mtendakazi badala ya mhepakazi? Nashukuru kusikia kuwa ulisema umejitolea kuwaunganisha makomredi, lakini maneno hayajengi ghorofa. Nakuomba upige mbizi: hadi kwenye hazina ya MUSO na ushone palipotoboka. Piga mbizi, uhakikishe kuwa kila aliye chini yako anawajibikia maagizo ya kikatiba. Mtihani wa kwanza ni jinsi utakavyochuja na kumteua Mhariri mkuu wa MUSO (Editor-in-chief). Je utafanya kama watangulizi wako gizani ama utaweka mambo wazi?. Anza mapema, enda na uchao si utwao.
MWALO REMMY katibu mteule wa makomredi. Mtetezi wa katiba ya MUSO. Unajua kuwa wapo wengi waliomwahidi komredi kuwa atapata katiba mpya pindi tu waingiapo madarakani. Kwenye uongozi wa hivi punde, yamkinika kuwa OLIVER BILL alipiga hatua kubwa ya kukarabati katiba lakini hakufua dafu. Labda atasingizia muda mchache mamlakani au upungufu wa raslimali. Au pia, atasingizia wadhifa wa mkate nusu. Ikiwa ni hivyo basi, ni aula ikiwa katiba hiyo itawachwa iwe jinsi ilivyo kwa kuwa, ukarabati huo umekuwa ndoano ya kuvua pesa za komredi na kuzimimina kwenye mifuko ya marafiki zao na bila shaka bosi mwenyewe. Najua kuwa mja hachagui zawadi, lakini wewe ulichagua huu wadhifa. Ulitaka uwe mti pajengwako kiota cha katiba ati. Nakuomba uzame : utafute alipokwamia OLIVER BILL na uweke kituo kwa harakati hizo. Funga asasi zote ambazo hujigamba kuwa zinakarabati katiba ilhali shabaha ni kumfyonza komredi na kupuliza ziliponga'ata kama panya. Kisa! Komredi ni mpita njia tu na iwapo humfai kwa haraka, utamfaa lini? Isitoshe, katiba haikarabatiwi kwa siku moja. Muda wako, kama watangulizi wako, ni mchache. Ushujaa si kupigana na akushindaye. Tekeleza majukumu yako mengine kwa kuwa, katiba mpya umekuwa wimbo wa kualika pepo mbaya afyonzaye pesa za komredi.
Si muhali kutaja kuwa mlibebwa na jamii. Na ya kuwa, mlitumia hela kuwarai watu kuwaunga mkono, lakini kumbukeni kuwa safari ni hatua. Mpe komredi cha kumfanya atabasamu. Uongozi usikuchafulie jina kwani, udandao pia, ndio ukubwagao.
No comments:
Post a Comment