ONLINE

Wednesday 15 June 2016

' ELDERS' ; ALHANI YA KIFO


'Elders' ni msimbo ambao wengi wa wanafunzi wa chuoni hutumia ili kurejelea wanafunzi walio katika mwaka wao wa nne. Mara nyingi, msimbo huu, iwe nyumbani au chuoni, huambatanishwa na heshima fulani kwa yeyote anayerejelewa. Wakuu, kama ilivyo katika kiswahili, ni waamuzi wa maswala nyeti katika jamii na pia huaminika kuwa radhi zao, ni fimbo. Ndiposa waswahili husema, asiye sikia la mkuu huvunjika guu. Uamuzi wao ati, ni wa mwisho na unaopaswa kufuatwa hivyo kwa wengi, umri na tajiriba ni istihaki kwa yeyote.

Mambo ni tofauti katika vyuo. Wakuu hawa hutumia ukuu woa kujitakia na kuwatakia wanaowaenzi makuu. Wanatumia ukuu huu kama kitega uchumi, kichinjaudhia kwa matatizo yao na pia kijikanzu jeupe cha kufunika weusi wa tabia na fikira zao. Wanadai kueleka mzigo wa jamii ingawaje kwao, jamii ni zigo la mlo,halilemei. Misimu ya uchaguzi huwa ndiyo muhimu sana kwa elders. Kwa yeyote ambaye tangu mwaka jana hajakanyaga chechele, atakumbukuka kuwa uongozi wa MUSO ambao upo mamlakani kwa sasa, ni zao la ukiritimba wa elders ambao baada ya kupewa kitu kidogo, wengi wao kama si wote walihiari kutoa kafara wagombezi wanaofaa na kisha kutupa kunguru wanaokula kila kitu, wasisaze hata harufu. Elders, ni kama izraili wenye uwezo wa kufisha azma ya kiongozi bora mwenye utendakazi na badala yake kumkumbatia kiongozi mwenye asali mdomoni na shubiri mkononi. Akila yeye asali, sisi anaturambisha shubiri. Yamkinika kuwa, hawa wapuza kwa jina elders hupewa kitu ambacho si kiubwa sana ili wawaidhinishe watu fulani kwa nia pia ya kupata mgao wa pesa anazolipa komredi, ikiwa watu walioidhinishwa watapokezwa fimbo ya uongozi na wanafunzi wa chuo.

Wagombea mbalimbali kwenye uchaguzi wa mwaka huu wameingiwa na kiwewe kutokana na msimbo huu wa elders. Licha ya kuimarisha umaarufu wao, hawana hakikisho rasmi kuwa watateuliwa kupeperusha bendera kwenye vyeo wanavyoazimia. Ikumbukwe kuwa, kutokea mwaka wa 2014,majina ya wagombea fulani yalikuwa hewa ya anga ya chuo hiki na kadiri muda ulivyozidi kusonga,majina hayo yalimiliki na kutamalaki masikio ya kila mmoja. Lakini mambo yaligeuka muda mfupi kabla ya uchaguzi wenyewe ambapo wamiliki wa majina hayo walilazimishwa kuondoka kinyang'anyironi na kuwaachia wengine ambao aidha walikuwa na mifuko mizito au majina yao ya pili yalitamkwa kwa namna fulani maalum. Nyote mnakumbuka Mwalimu Don Owino na Eugene Muchai ambao kabla uamuzi wa elders, walikisiwa kuwa huenda wakawa uongozini. Lakini kwa ajili ya ulofa na matamshi ya majina yao ya pili, radhi za wazee ziliwakwepa. Wakasalia chui, waliong'olewa meno na kukatwa makucha.

Lakini pia, tusimlaumu mwewe ilhali kipanga yuwesha vifaranga. Sisi wanafunzi wa vyuo tumejigubika kwenye blanketi zito la Ukabila na kulala usingizi usioelezeka. Ikiwa tutamakinika na kutambua kuwa, sisi ni kama wao na tofauti tu ni maeneo na utamaduni wetu, basi ugumegume huu elders hautatuponza kamwe. Ujumbe kwao ni kuwa; mngakaanga bizi, tu chini ya gae tunawatazama, hivi karibuni huenda chura wakamwangusha tembo.

No comments:

Post a Comment