ONLINE

Friday, 27 May 2016

Kurunzi ya Ligi ya Mabingwa



Na Yassina Terry

Jumamosi hii, kivumbi kinatarajiwa kule San Siro mwendo wa saa nne usiku, huku miamba wa Uhispania Real Madrid na Atletico Madrid wakitoana kijasho. Wengi wametabiri kuwa Atletico Madrid watalitwaa kombe hilo kutokana na itikadi ya hivi majuzi kuwa timu yoyote inayoiondoa Barcelona, hutwaa Kombe hilo la Mabingwa. Hata hivyo, Jukwaa la Michezo linaangazia kwa kina zaidi historia ya timu hizi mbili na uzito wa fainali hii hatua kwa hatua.

Timu hizi mbili zilikutana mara ya kwanza mwaka wa elfu moja mia tisa ishirini na nane katika michuano ya Copa del Rey, mechi ambayo Real Madrid waliwacharaza Atletico Madrid mabao matatu kwa nunge. Wapinzani hawa wamekutana hivi karibuni katika michuano ya La Liga mwezi February mwaka huu, mechi ambayo Real Madrid walipoteza kwa Atletico Madrid bao kwa bila.

Ushindi mkubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa kati ya timu hizi pinzani, ulikuwa ushindi wa Atletico wa mabao matano kwa nunge dhidi ya Real Madrid msimu wa elfu moja mia tisa arobaini na saba na arobaini na nane katika michuano ya La Liga. Hata hivyo, Real Madrid walivuna ushindi kama huo wa mabao matano kwa nunge dhidi ya Atletico Madrid msimu wa elfu moja mia tisa hamsini na nane na hamsini na tisa na ule wa elfu moja mia tisa themanini na tatu na themanini na nne mechi zote zikiwa za La Liga.

Wawili hawa wamecheza jumla ya mechi mia mbili kumi na mbili, huku Real wakipata ushindi mara mia moja na saba na kutoka sare mara hamsini na moja. Atletico wamepata ushindi mara hamsini na nne. Jumla ya mabao yaliyofungwa na Real Madrid ni mia tatu hamsini na tano huku Atletico Madrid wakifunga jumla ya mabao mia mbili sabini na moja.

Timu hizi aidha, zilikutana katika fainali za ligi ya mabingwa mwaka wa elfu mbili kumi na nne kule Lisbon, mechi ambayo Real walipata ushindi wa mabao manne kwa moja baada ya muda wa mazidadi. Walipatana tena katika robo fainali za UEFA msimu uliofuata ambapo walitoka sare ya kutofungana kule Calderon na baadaye Real wakapata ushindi wa bao moja kwa bila nyumbani Santiago Bernabeu.

Wapinzani hawa watakutana tens wikendi hii katika fainali za UEFA kwa mara ya pili kule San Siro. Usikose kushuhudia kivumbi hicho.

No comments:

Post a Comment