ONLINE

Saturday, 28 May 2016

DADAVUO LA SIASA ZA MUSO





Mwenye macho haambiwi tazama, Hali imeanza kubadilika chuoni.Kila kuchao makundi mbalimbali yanaendelea kushuhudiwa katika maeneo mengi chuoni. Hii ni ishara tosha ya mchakato mzima wa siasa kung’oa nanga .Wanaojumuika katika makundi haya madogo madogo si wahubiri, si wapiga mtindi, si watafiti bali nitawaita wakeretwa  wa kisiasa.

Njiani kunashuhudiwa salamu zisizo kifani. Ikilinganishwa na muhula uliopita pana ongezeko la salamu za mja maradufu. Inakisiwa kuwa wale wote walioongeza ukuruba wa salamu ni wagombea wa nyadhifa aula katika jaramandia la MUSO. Kwao, hii ni njia kabambe ya kuwateka bakunja waja katika familia ya wapiga kura ili kuonyesha undugu walio nao na kupata uungwaji mkono. Tukumbuke undugu ni kufaana....
Baada ya kupiga kura natumai pia hali hii itaimaarishwa, nitakuwa mchache wa fadhila ikiwa zangu kongole sitawapa kwa ukengeushi huo. ‘Wangwana,waheshimiwa,ungana nami katika mchakato mzima wa kupiga msasa usemi “mgema akisifiwa tembo hulitia maji” na kuufanya kinyume kwa matendo.

Mtandaoni pia kazi inapangwa na kupangika.Mkesho umeanza mapema na ngoma inasakatwa kwa mirindimo ya kila aina.Ukweli unabadilishwa kuwa uongo na kinyume pia.Mawakala wa kisiasa wanapewa mjazo wa simu ili kuiteleza kazi hii. Kauli mbiu imesalia hakuna vya bwerere, “no mercy” “tibbim” “no symphathy votes”ndio wimbo wa kila siku.Waja hawa wana tajriba ya juu zaidi ya kucheza na maneno na kuwafanya “waheshimiwa” kujistaha na kuuona ushindi viganjani mwao. “Tunangoja tu kutawazwa uongozi,”ndio baadhi ya maneno matamu yanayomtoa nyoka pangoni....usiniulize nyoka ni nini maanake mnajua.Ukweli ni kwamba ndoto hii kwa wengine itasalia kuwa ruwaza maanake ni lazima pawe na mshindi mmoja na  hii itategemea na mikakati ya mtu binafsi.

Mtindo wa mavazi pia umebadili kwa wachache ili waonekane “waheshimiwa” bali siyo wenye miwa.Koti, tai na kaptura zilizonyooka utadhani mlingoti wa bendera  kutokana na pasi kuwa kiungo cha kila siku. Wanadai pia mavazi ni kigezo cha kuzingatiwa katika kuwachagua viongozi chuoni....hili wapiga kura mtanijibu baadaye.

Nyadhifa zilizotengewa kina dada hususan wadhifa wa naibu mwenye kiti na mkurugenzi wa masuala ya maakuli zimeshuhudia wagombea wengi.Dondoo zinadokeza kuwa wengi wao wamo katika shindano la urembo kisio ambalo wao wanalipinga.Kwa mujibu wa historia urembo umetumiwa kama kigezo cha kuwachagua kina dada haswa na timu tukufu “mafisi sacco” kumbukeni ashakum  si matusi.Hali ilivyo sasa kina yakhe watapata wakati mgumu kutokana na vipusa hawa walio watia wengi mbioni ukipenda mawindoni.Labda miungano ya kijamii kama ilivyo destrusi itakusuru nafsi ya baadhi yao ili wauone “ufalme” wa MUSO.

Kuna wale wagombea ambao kwa sasa wameyaficha makruhu na kubadili ngozi zao zilizo na hulka za chui kuwa za kikondoo. Hawa ni watu hatari ambao baadaye wataisifu methali asante ya punda ni mateke.Inahitaji makini kutambua vibaragozi wa aina hii ili baadaye tusije kuungama na kusaga meno kwa kusahau wosia “majuto ni mjukuu huja baadaye”

Kwa wasomaji wagombea wengi bado waja wamo pangoni katika windo la kukusanya mapeni ya kuwatilia chambo.Wengine wamo katika majaribio tu  na nia mbovu za kutaka kulipwa ili wawaachie wapinzani wao fursa ya kuwania viti mbalimbali.Ni jukumu la wanazuo watukufu kuwapiga msasa wagombea wote bila kujali kabila, jinsia na hata uwezo wa kiuchumi  ili kutambua ufaafu wao na kukinusuru chombo.Baadhi yao wana nia fiche isiyo na umuhimu kwa jamii kubwa ya wanazuo.

Jambi langu litalikunja siyo kwa ukosefu wa wino bali ngoma ikipigwa sana hupasuka.Tuzingatie utu katika kampeni zetu  bila kusahau ni suala la mpito tu lahaula mtu akikosa utu, kutu huingia na kumfanya mtu kuwa butu.

No comments:

Post a Comment