ONLINE

Monday, 30 May 2016

AKUFUKUZAYE HAKWAMBI TOKA


Waama, ni dhahiri shahiri kama jua la utosini kuwa, anayekufukuza si lazima anene neno ‘toka’ ila utaona kwa vitendo.Ingawa ni jambo la hasidi sana mtu kutokwambia hataki mambo yako na akuelekeze tu kuwa nyumba yake uione paa, hilo ndilo jambo la maana kuliko mtu kugundua mwenyewe kuwa hahitajiki au kuwa yeye ni jipu katika maisha ya mwengine.

Mapenzi yanatawala dunia jinsi tunavyojua .lakini katika kila penzi ,huwa na vikwazo na ni kutoka kwa hivyo vikwazo ndipo watu huunda minyororo ya mapenzi.Sisi kama wanadamu wenye akili razini ,tunafaa kutumia akili zetu si tu kwa kufikiria jinsi ya kulisukuma gurudumu la maisha yetu, bali pia kufikiria kitu ambacho mwengine anafikiria sana kuhusiana na matendo yako.

Vitendo ni muhimu sana hasa kwa walio katika uhusiano wa kimapenzi.Anayetaka kumaliza uhusiano wa kimapenzi hatokufungulia mlango akwambie amechoka nawe. labda tu kama ni mwenye ujasiri usiowasirika

Kuna tabia ambayo waja wengi huwa nayo na mwenzangu, usimake wala kuhangaika na kubung’aa.Ni tu ukweli mchungu  unaofaa kukubali.Akina dada,ukiona dau linaenda mrama,shuka kabla hujashushwa na kuaibika.Huyo mwanamume unayemuenzi akianza kukupuuza, usilie wala kuona ulimwengu umekusaliti,jikakamue na uondoke rawsababu hiyo ni njia yake ya kukuambia uhame.

Kitambo ulikuwa ua la waridi,hurulaini wa peponi, wakati mapenzi yalipoanza. lakini baada ya muda wewe umekuwa si chochote .Hiyo ni njia bayana ya wewe kugura katika huo uhusiano.Kama unangoja kengele ama filimbi ndiposa uondoke,pole.

Kaka,umeona tu vizuri katika mtandao wa kijamii;katika whatsapp,instagram na kadhalika picha anazoweka ni za mwanamume mwengine;si babake,si kaka yake na ukimwuliza ,neno atakalotamka ni ‘rafiki’.Upuuzi wako utakufanya uamini.Picha yenyewe imewekwa kwa muda na picha yako hawezi dhubutu kuiweka.Huoni anaaibika kukuweka wewe na kuwa chaguo lake liko kwingine!Hama kaka

Umeona simu yake na mawasiliano yake si ya kuridhisha.Mtu anayedai anakupenda anawezaje kumtumia mwengine arafa za mapenzi halafu wewe huyo umeridhika naye!Unaambiwa toka lakini sababu umezoea maneno na si vitendo, utajikalisha hapo.Tunafaa kutilia manani vitendo zaidi ya maneno.Msome mtu vizuri na ujue matendo yake vyema na uyatafsiri mwenyewe sababu: akufukuzaye, hakwambii toka, ila utaona kwa vitendo vyake.

No comments:

Post a Comment