ONLINE

Wednesday 2 March 2016

UKISHIKWA SHIKAMANA

Bw. JOMO SAMUEL

By JOMO Samuel
        Hayawa hayawi huwa,hatimaye siku iliyoongojewa sana na wanafunzi wa Kitivo cha Elimu ilitimia.
        Maandamano ya wanagenzi hawa yaling'o nanga nje ya ukumbi wa wanafunzi.Kinara wa masuala ya elimu Bwana Jairo Moses aliwahakikishia uwepo wake na kuwanasihi wanazuo hao kuandaa maandamano ya amani.Alisema kuwa ni lazima masuala yao yaweze kujibiwa bila kupoteza muda.
        Bwana Jared Mogire,Oliver Bill,Elvis Langas na viongozi wengine hawakusazwa.Walionyesha umoja wao kwa kuungana na wanazuo hao waliokuwa na hamaki zisizo kifani.Waliwaondoa wanafunzi wote waliokuwa katika majumba ya mihadhara waandamane na kuimba nyimbo waama,umoja ni nguvu utengano ni udhaifu.
        Wanafunzi hawa walilalamikia masuala yafuatayo:
    1.Wahadhiri kutoa utathmini kwa wanafunzi walio nyanjani.
    2. Kucheleweshwa kwa matokeo ya mtihani kwa wanafunzi wa mwaka wa pili na wa tatu.
   3. Kutofunzwa kwa kozi za kimsingi.
   4. Wanafunzi kutozuru nyanjani kimasomo.
   5.Ukosefu wa vyumba vya kutosha vya mihadhara.
   6. Ukosefu wa vifaa vya kufanyia majaribio kwa wanafunzi wa masomo ya sayansi.
        Wanazuo hao walionyesha hamaki zao kwa kuimba nyimbo mbalimbali zikiwemo "Walimu msilale,bado mapambano,bado mapambano." Bendera ya chuo iliteremshwa nusu mlingoti ishara ya maombolezi.Hatimaye mlingoti wa bendera hiyo ukang'olewa.
       Iliwalazimu wasimamizi wa chuo kuandaa mkutano wa dharura ili kuafikia majibu mahususi na kuidhibiti hali.Kupitia kwa memo,Profesa Nathan Ogechi aliwahakikishia wanafunzi hao kuwa wenzao walio nyanjani wataanza kufanyiwa utathmini kuanzia Jumatano wiki hii.Matokeo ya mtihani yatatolewa kuanzia Jumanne tarehe moja,na wanafunzi wote waliolipa pesa za kuzuru nyanjani wataenda bila kupingwa.
       Aliahidi kuwa masuala mengine yatashughulikiwa ipasavyo na suluhu ya kudumu kupatikana.
       Kilicho na mwanzo hakikosi mwisho hatimaye maandamano hayo yalifikia ukingoni na kila mmoja kurejelea shughuli zake za kawaida.

No comments:

Post a Comment