ONLINE

Friday 11 March 2016

MAHABA YA CHUONI



Tulipokuwa bado malimbukeni wa maisha, wazazi wetu walitumotiisha sana ili tutie bidii masomoni ndiposa tupate fursa ya kujiunga na chuo kikuu. Zaidi ya hayo, tuliambiwa chuoni tungepata mke au mume mzuri ingawa yasemekana wema hawajazaliwa. Wengine kama mimi tuliamini,wengine labda hamkuamini ila bado mlishikilia dhana ya kuja chuoni na kando na shahada, upate pia mwenzi wa roho. Hilo litafanyika?

Dhana ya uhusiano kati ya ghulamu na gashi kwenye vyuo vikuu imefungamanishwa na vitendo vya ufuska kwa sana kiasi kwamba mkataba kati ya hawa wapenzi wawili huwa na kifungu kikuu cha ruhusa ya haki za ndo aghalabu kuonyesha huba eti. Chovya chovya humaliza buyu la asali hivyo baada ya cheza cheza nyingi, uhusiano huo hukatikia pabovu baada ya kufifia kwa hamu na utamu wa asali yenyewe.Hili limewafanya wanazuo wengi kuvumbua wazo kuwa uhusiano wa vyuoni ni moto wa karatasi tu, huzima baada ya muda mchache. Labda ni ukweli, labda uwongo, labda ni utani.

Mkamia maji hayanywi;waneni walinena. Pupa ya wanagenzi ambao wamepata uhuru kwa mara ya kwanza ndiyo chemichemi hasa ya kufa kwa uhusiano huu. Pupa hii imekuwa mama ya wanazuo wengi kuwekwa kwenye kategoria ya team mafisi. Huwa na tamaa ya kula chochote wakionacho, kiwe kibovu au hurulaini. Hawajali, hawabali. Lakini sidhani kwamba, hili linatosheleza dai la kufeli kwa uhusiano wa vyuoni?

Fikiria kuhusu mkulima wa nafaka, tuseme mahindi. Iwapo mkulima huyu atayaona mahindi kuwa chakula, ataelekea kwenye kinu asage unga . Akiyaona kama milki ya kumfaa baadaye, atayapanda kama mbegu ili azalishe zaidi au ayahifadhi. Ni sawia na unavyomwona mwenzako chuoni, ukimwona kama kidimbwi cha kuogelea, utapiga mbizi. Ukimwona kama mtu atakayekutunza hapo baadaye na kukuzalia labda, badala ya kumla, utazidisha mapenzi. Sioni kisichowezekana.

Najua ushujaa si kupigana na akushindaye lakini ninaamini yawezekana. Yawezekana kuchumbiana kutoka chuoni hadi kufunga pingu za maisha. Naam, Yawezekana; ijapokuwa itategemea iwapo utabadilimtazamo wako kuhusu yeyote ambaye mna uhusiano wa kimapanzi. Itategemea pia jinsi ulivyokuzwa, iwapo ulikazwa sana na wavyele kiasi cha kunyimwa uchangamano, sina uhakika kama utafaulu kutotumia kikamilifu fursa utakayopata mkiwa wawili chumbani. Pia itategemea na shughuli zako chuoni ;kupapasa Bibilia au Kurani, kuisoma na kuelewa Bibilia au Kurani na mwisho kupenda kuingia vyumba vya burudani kama vile F2 na dunda kwani mtama ukiwa mui sitaraji wapishiwawe aula. Pia itategemea marafiki zako, ikiwa ni viruka njia basi usijitie hamnazo kumbuka gome la udi, si la mnuka uvundo. Kwa mihili hiyo, natarajia kuwa umebaini hatima ya uhusiano ulionao na yule dada au kaka. Je uhusiano wa vyuoni ni moto wa karatasi au umeme unaodumu? Hewala. 

No comments:

Post a Comment