ONLINE

Friday 26 February 2016

WIMBO MPYA WA TAIFA

.....Licha ya kufeli kutimiza manifesto.....kuna mengi ambayo si machache alioitimiza....

By WANYONYI Simiyu

Rais Kenyatta a'li hai
Uhuru wa nchi hii uliopatikana kwa kumwagwa damu na kuwakosesha usingizi wazee wetu ni hatuaya staha ambayo kila mwananchi anafaa kusherehekea. Kucharazwa kwa wimbo wa taifa ni ishara moja ya kusherehekea huko kando na kuipeperusha bendera ya taifa. Mkenya yeyote anayejitoa kwa mambo haya mawili ni mwenye uzalendo.

Ni jambo la kutia hofu kuona mwelekeo wa nchi ukibadilika na kuchukua mkondo mwingine. Lalama miongoni mwa viongozi na hata wananchi wengi zimeipa nchi hii sura nyingine ukilinganisha na hapo awali. Serikali imebadilishwa na kuwa mbeba lawama. Ugatuzi ukidorora kutokana na matumizi mabaya ya mgao wao na magavana, maseneta na wabunge wote hulaumu serikali ya rais Kenyatta kupitia kwa wizara ya ugatuzi kuwa inahujumu ugatuzi. Ama kweli, mabaya ya bwana si mazuri ya Juma kitwana. Serikali ya rais Kenyatta imegeuzwa na kufanywa ng'ombe wa mkata ambaye hashiki mimba, akishika hazai na akizaa, hazai mapacha. Imefanywa kama ng'ombe ambaye hutoa maziwa meusi.

Uzalendo pia umehajiri nchini. Ni jambo la kufisha moyo kumsikia Gavana wa gatuzi fulani nchini akipendekeza kuondolewa kwa picha ya rais katika afisi zote za magavana wa mrengo wa CORD na badala yake iwekwe picha ya waziri mkuu wa zamani bwana Raila Odinga. Jambo liliosahaulika ni kuwa, Rais Kenyatta ni kiongozi wa Kenya bali siyo kiongozi wa muungano wa makabila. Hata hivyo, uongozi ni zamu. Fikiria siku moja Gavana huyo araukie habari kuwa mkewe amemwasi, akatupa pete ya ndoa na kufunga ndoa upya na jirani anayepakana naye. Au siku moja, bwana Raila awe Rais wa nchi nao viongozi wa mkoa wa kati waape kutoweka picha yake kwenye afisi za kitaifa. Ni jambo linaloonyesha ubinafsi wa viongozi wetu, siyo tu kwa kujitakia makuu, bali hata kutanguliza chuki ya kikabilana kimaeneo.

Nawakumbusha wote wasio mheshimu Mstahiki Rais kuwa, uongozi ni zamu na ukipanda ngano magugu pia hutokea ili kuchochea kupalilia lakini ukipanda magugu hutaiona ngano ikiota. Kama wasemavyo waswahili, akutendaye mtende bali mche asiyekutenda

Chui hata awe mkali kiasi kipi, ana mke na wanawe wanaocheza naye. Sawia na Rais wetu, licha ya kufeli kutekeleza ahadi za manifesto ya JUBILEE, angalau kunayo mengine ambayo si machache aliotimiza. Mgala mwue eti, ila haki yake umpe. Lalama zisizo na suluhu ni mfano wa raia aliyejivika nguo za polisi na kujiona kama polisi. Akawafumba macho raia wenzake kwa majisifu na vitisho ila aitwapo kuwa kuna uvamizi umetokea, hukimbia hadi kwenye chumba chake cha kula na kuanza kupiga mayowe ya serikali saidia,serikali saidia. Kama ilivyo, zindiko la mwoga ni kemi na alalamikaye sana hana maendeleo.

Taamali
Kuregarega si kufa, kufa ni kuoza utumbo-tusimzike, Rais bado ali hai.

No comments:

Post a Comment