ONLINE

Friday 26 February 2016

JUMATATU 29: TUPE HAKI YETU


By JOMO Samuel

        Ngoja ngoja huumiza matumbo."Tumengoja...,""Tumevumilia....,""Tunaumia...na tumechoka."Punda amechoka," ndio kauli mbiu ya wanafunzi wa Kitivo cha Elimu mwaka wa tatu.

Wanafunzi wa Kitivo cha Elimu hususan wale wa mwaka wa tatu hapa Chuoni wanalalamikia utepetevu na kutowajibika kwa baadhi ya washika dau Kitivoni.Wanaofanya somo la jiografia wanadai kuna kozi ambazo tangu semista ianze hawajafunzwa la ajabu wanatarajia kuufanya mtihani wa kozi hiyo mwisho wa muhula.Kozi yenyewe ni ya Utalii na Usafiri. Mhadhiri anayestahili kufundisha kozi hiyo wanasema amepanga na kupangua siku ya mihadhara yake si jumatatu...si Jumanne....si Jumatano...na huu umesalia mchezo wa danganya toto jinga.

Kuhusu matokeo yao wanasema si ya mtihani bali ya mitihani.Wanafunzi wa mwaka wa tatu ndoto zao za kupewa matokeo kabla ya tarehe kumi na saba mwezi huu zimesalia kuwa ruwaza...labda subira huvuta heri ingawa baada ya subira heri hawajaiona.

Duru za kuaminika kutoka kwa katibu mkuu wa muungano wa wanafunzi katika kitivo cha Elimu Bwana Ojwang ni kuwa wanakitivo cha Elimu na wale wa kitivo cha Sanaa na Sayansi za Kijamii wamebaki kulaumiana kwa kuchelewesha matokeo.Haijulikani mhusika mkuu katika drama hii ni nani....?waama fahali wawili wakipigana nyasi ndizo huumia.

 Kutokana na masaibu haya wanafunzi wa Kitivo cha Elimu wote kwa pamoja chini ya "Sossion" wao Bwana Ojwang wameamua na liwe liwalo.Wamemwandikia naibu chansela mwandamizi wa masuala ya elimu waraka na kumtaka kulishughulikia suala hili kama suala la dharura.Wanazuo hawa wanataka suluhu ya kudumu kabla ya jumatatu saa mbili asubuhi la sivyo hawatakuwa na budi kuuchukuwa mwelekeo ambao kwao watauona una ufaafu.

Siku ya Jumatatu...Siku ya Siku....Siku ambayo wanagenzi hawa wanasubira kwa matumaini kuwa watapata kilicho chao kwa vyovyote vile.Watajumuika katika ukumbi wa LH1 na kuafikiana kwa kauli moja mwelekeo watakaouchukuwa. wasemavyo akina babu, umoja ni nguvu utengano ni udhaifu.

No comments:

Post a Comment