Wapo washika ngazi na wapanda ngazi. Mwanzoni, wote ni binadamu. Wenye haki sawa, uwezo sawa na bila shaka huwa marafiki. Urafiki wa mche na kinu hasa. Mmoja akiponda, mwingine atazuia hasara eti. Wote hudhaniwa kusafiri kwenye safu sawa ya anga ingawa kila mmoja huwa na nyota yake. Sasa, hili la nyota ndicho kibainishi cha hawa wawili. Nyota ya mmoja huonekana iking'aa wakati wa safari huku ya mwingine, licha ya kuwa haizimi,huwa hafifu hadi kesho. Wakati mwingi mimi hujiuliza. Mbona nyota hizi mbili husafiri pamoja, kwenye anga sawa na hali sawa ya hewa ilhali moja hunang'anika kuliko nyingine? Zamani, nilidhani hilo ni swali la kitashtiti. Lakini kumbe sivyo. Ipo sababu. Lipo jibu, tena kubwa kuliko ndovu wa sahara na bayana kuliko usiku wa mbalamwezi. Yaani ni jibu linaloonekana wazi ingawa kwetu binadamu, ukubwa wa gololi, si kigezo cha kutathmini uwezo wa mtu kuona. Siyo kila gololi ina mboni na siyo kila mboni ina uwezo wa kuakisi mwangaza vyema. Kwa wale wote wenye matatizo ya kuona ijapokuwa kuwa wana mboni na gololi, basi sikilizeni sababu hizi.
Mwanga wa nyota hizi siku zote hutegemea uwezo wa wamiliki wake kuwaza kama jua. Fikiria, nyota hazionekani mchana. Lakini jua huhakikisha kuwa nyota hizi, licha ya kutokuwepo wakati huo, wananyonya mwanga wa kutosha ndiposa jua likufapo mawio, anga izidi kuangazwa usiku. Kwa lugha nyepesi, jua husaidia nyota kupiga makasia ili ung'avu wake uonekane. Lakini nimegundua kuwa, nyota hii ambayo ni hafifu, huwakilisha ukubwa wa kitu, mtu au jamii kiumbo hasa, lakini uzani hamna. Kuu kwake ni kubururwa tu. Hata matrela afadhali. Mkokoteni hasa. Bila kubururwa na mtu, punda, maksai au chochote chenye nguvu, hausongi. Labda kwa kukosa nguvu, maono au pia mazoea tu ya kubururwa tangu asili na fasili. Pia labda raha ya kusafiri na kujigamba kwa nyota ya mwenzi iliyokando ya yenu na ambayo inang'aa.
'waona sasa, hao hawawezi bila sisi. Na kwa kuwa funika hailingani na iliyo wazi, tushabikie hii iliyo wazi ijapokuwa moyoni tutaificha hii yetu iliyofunikwa. Angalau hili litatuepushia vicheko na masimango eti kuwa sisi ni yatima wa kisiasa'. Doh! Nguo ya kuazima haisitiri matako! Mtafunzwa hadi lini? Wakati wao wanajitahidi kumfanya wao awe maarufu, nyinyi mnaotea tu, kama mwewe mnangoja umaarufu wake ushike kasi. kusafiri kwa nyota ya wenzi wenu ndiyo raha yenu. Lakini nguvu zenu ni sawa na pia wingi wenu ni sawa na mchanga ufuoni. Mbona msitumie uwezo wenu kuchochea mwangaza wa nyota yenu!
Msambaratiko! Kumbe wingi wa mchele kwenye gunia pia ni wingi dume ndani. Humo! Mmegawanyika vipande vipande hadi kuunganishwa, hata shazai haiwawezi. Kisu ni kimoja. Lakini ni upande upi wa kisu utanolewa. Kila jamii inang'ang'ania kutia makali upande fulani. Baadaye, kila upande wa kisu hicho kimoja huwa machinjio. Mnaishia kutumia paka wawili kumfukuzia panya mmoja. Mna uhakika watamshika yule panya! Wakati wao wanajenga daraja dhabiti, nyinyi mnajenga kuta za saruji kati yenu.
Mwishowe mambo huwa tenge tahanani. Washika ngazi ndiyo cheo chenu. 'muungano muungano. Kichango kuchangizana.' mtachanga nini na mifuko mmeitoboa. Kumbuka :mshika ngazi, hupigwa teke mdomoni. Ikiwa kwa msambaratiko huu, mtazidi kutumaini kuwa mpanda ngazi hushuka, mtasota saaana!
No comments:
Post a Comment