Na Dickson Matiabe
Watoto huimba
Kwenye hivyo vibarabara
Taratibu vilivyobeta
Kisha kuhadithana
Hadithi ya vile vidazi
Walivyokula asubuhi
"Esuguku"
Ndivyo wanavyoiita siku hii
Siku mpya ya shani
Leo Bosibori yumo njiani
Ili akamwazime Moraa unga
Ili akawapikie wanawe vidazi
Katika siku hii mpya
Ambapo watasahau unywaji uji
Kisha atamsimulia kule kisa
Cha mumewe kutoweka nyumbani
Na kisha kunyapia nyumbani
Usiku wa manane
Usiku wa kiza totoro
Kwenye hivyo vibarabara
Vinavyobeta taratibu
Wazee wa kesho watapita
Kwa yao mingi mikogo
Huku vicheko
Vya dhihaka kuvipasua
Wakiicheka ile kesho
Iliyojificha kwenye vilima vile
Waonayo yaja wala haiji
Huku wakizungumza
Lugha yao ya kishetani
Kisha katika Siku hii
Watakua wamesahau
Hadithi ya yule kinyonga
Aliyepita kitongijini
Na kuwatemea watu mate
Ila, jua magharibi
Taratibu linapotua
Navyo videge kurejea viotani
Watakuwa wameshaingia mtegoni
Kwenye hayo makutano ya njia
Wazee wa juzi watakutana
Na vijiredio vyao mkononi
Kisha Kwenye hivyo vijabali na vijiwe
Polepole watajilisi
Huku wakisalimiana
Kwa mikono yao dhaifu
Kisha watakumbushana
Nyakati zile awali
Nyakati zilizo tamu
Walipowakamata swara kwa mikono yao
Kisha wataulaani wakati
Wakati uliodinda kushikika
Na kisha baada ya kukikata kiu
Watajikokota vyumbani mwao
Na kuliacha likazidi kutawala.
No comments:
Post a Comment