ONLINE

Monday, 7 March 2016

SIKU NJEMA KWA WANAZUO WA KAUNTI YA KAKAMEGA


By JOMO Samuel

Ilikuwa ni siku ya furaha na nderemo kwa wanazuo wa hapa Moi wanaotoka kaunti ya Kakamega walipozuru bwawa la Kesses.
         Wakiongozwa na Mwenyekiti wao Bwana Nahashon Oduor Milton walitia nanga katika uga wa Bwawa la Kesses mwendo wa saa nne kwa shughuli za mandhari
         Wanazuo hao walidhihirisha ucheshi wao kwa kuimba na densi za chini kwa chini.Waliimba nyimbo za kitamaduni za kiluhya,walinengua viuno na kusisimua mabega kiasi cha haja.Michezo mbalimbali ukiwemo mchezo wa kuruka kamba pia haikusazwa na kujikumbusha enzi za utotoni.
          Ngoma ikipigwa sana hupasuka,hatimaye wanagenzi hao walitulia kivulini ili kuzungumzia baadhi ya agenda za siku.Bila shaka ilikuwa ni siku ya kujuana na kufurahia kwa pamoja.Kila mmoja alielezea furaha yake na imani alio nayo kwa viongozi wa muungano wao ambao kwa mara nyingi wameonyesha kuwajibika kwa majukumu yao.
         Nahashon Oduor alisema kuandaa mandhari hayo ilikuwa ni njia mwafaka ya kuwaleta wanazuo hao pamoja.Aliwasihi wawe na umoja na kusaidiana katika changamoto mbalimbali zinazowakumba hapa Chuoni.Alisisitiza ni bora kila mmoja aweze kushika kadi ya kura kama njia ya kipekee ya kuleta uongozi utakaowafaa.Katika mazungumzo naye alibaini kuwa muungano wao uko imara na hapati ugumu katika uongozi wake kutokana na umoja na uhusiano mwema baina ya wanachama.Ameweka mipango kabambe kuhakikisha wanafunzi wote wanaotoka katika kaunti ya Kakamega wameweza kujumuishwa kwenye muungano huo.
          Julius Maube ambaye ni mwanagenzi wa mwaka wa pili hapa chuoni aliwazidishia ucheshi.Akisaidiana na mwenyekiti waliwapa wote vinywaji angalau wapanguze koo kwa udhamini wa Lydia Pamela Nyangala,almaarufu "Senje Lydia Pamela Nyangala omwana wa Papa Nyangala" ambaye kwa wakati mmoja amehudumu kama mtangazaji wa Mlembe Fm.Aliwasilisha ujumbe wake na kuwarai mabingwa hao wamuunge mkono katika kinyang'anyiro cha mwaka 2017 ambapo atawania kiti cha Mwakilishi wa wanawake,Kaunti ya Kakamega.Juhudi zimesalia kwa wanagenzi wa kaunti ya Kakamega kuandaa siku na kukutana naye ana kwa ana.Kupitia kwa njia ya simu Bwana Julius alizungumza naye na kumhakikishia kuwa yu tayari kuitikia mwito wao wakati wowote.
         Kilicho na mwanzo bila shaka hakikosi mwisho,shughuli za mandhari zilifikia kikomo mwendo, wa saa tisa alasiri kwa nderemo na vifijo ishara ya siku ya kufana.

No comments:

Post a Comment