ONLINE

Wednesday, 16 March 2016

WANADADA KATIKA SIASA NA UONGOZI WA VYUO VIKUU

Winnie Nyandiga akiwa anaapishwa kuwa Rais wa muungano wa wanafuzi wa MMUST


Tangu mwanzo wa karne ya 21 vuvuzela za kusawazisha haki za wake na waume zimekuwa zikisikika katika pembe za mabara yote ya ulimwengu.
Taifa la Kenya limeshuhudia wimbi la wanaharakati waliojitolea kwa vyovyote kutetea haki za wanawake katika asasi zote. Sisemi juhudi za vuguvugu la maendeleo ya wanawake hazikuzaa matunda kwa kumwona mtoto wa kiume bado “anatawala” katika jamii.

Licha ya kuwa katiba ya Kenya inampa mwanaume na mwanamke haki sawa katika uongozi,ukweli ambao ni mchungu unadhirisha kuwa asilimia kubwa ya wanawake wangali wanaamini na kusadiki kwamba madume ndio wenye vibali vya kuongoza!

Hatua ya wanafunzi wa chuo Kikuu cha Masinde Muliro ya kumchagua Bi. Winny Apiyo ni ya kuleta mwamko mpya kwa siasa za vyuo vikuu ambazo zimetawaliwa na ukoma wa udikteta na ubinafsi wa wanaume.Endapo Bi. Winny hakupewa kura kwa urembo na umbo lake la nambari nane,MMUST imeificha maudhui ya taasubi ya kiume iliyotawala sana katika fasihi za Afrika.
Kila historia ya wanasiasa au baadhi ya watu mashuhuri inapotajwa,ni kawaida kusikia ati nani kawa kiongozi wa wanafunzi alipokuwa chuo kikuu.Naam,iwapo hujui hata Rais wa Marekani Barack Obama alikuwa student leader siku zake za ujana.

Usiniambie akina dada hawapendi uongozi wakiwa chuoni eti kwa sababu wanashughulikia kilichowapeleka chuoni.Yaani wanasoma kwa bidii za mchwa ajengaye kichuguu kwa mate.Kwa hiyo mambo ya siasa ni ya ngoswe na waja husema mambo ya ngoswe mwachie ngoswe mwenyewe.
Wanaojua kusema husema kuwa uongozi wa chuo humwandaa mtu kuwa kiongozi wa taifa.Endapo warembo wa chuo hawataweza kujitosa siasani na kugombea uongozi wa vyuo huenda ndoto zao za kuwa na usawa wa kijinsia ukawa ule wa Alinacha.

Ni dhahiri kuwa hupewi uongozi kama zawadi ya maua.Ila hutafutwa kwa gharama yoyote.Wallah Bin Wallah asema inapatikana kilelebaba na sio kilelemama.
Wadaku wanashikilia kuwa kile mwanaume analoweza,mwanamke anaweza kulitenda vizuri sana.Kwa hiyo kama wanaharakati wa kiume wanaweza stahimili vitoa machozi wakati wa maandamano,akina Winny wanaweza stahimili milio ya risasi.

Kama” Babu Owino” ana uwezo wa kugharamia chakula cha cha wanafunzi wa chuo kikuu cha Nairobi katika hoteli ya kifahari ya Serena,kina “Wanjiku” wana uwezo wa kugharamikia maakuli ya mchana kwa wanafunzi wote wa vyuo vikuu.
Aise! Iwapo madume walio uongozini wanajua kunyamaza kwa kupuliziwa marashi ya pesa huku wanafunzi waliowachagua wakiliwa na kunguni,warembo wetu wanajua kujipodoa kwa pesa za comrades wasioweza kununua hata ARIMIS.

Vipi utakuwa gavana wa gatuzi la Nairobi ilhali hukumudu kuwabembeleza wapiga kura ukiwa chuoni.Kama ulijificha kwa sponsor wengine wakililia haki yao ,ni lini utawarai wakenya wanaojua kunyonya pesa na maneno matamu ya wanasiasa  wakupe kura ya kuwa urais?

Ni udikteta kuona miongoni mwa magavana 47,hakuna mwanamke kwenye baraza hili la marais wa kaunti ambao mdaku wanagu aniambia hula mshahara na marupurupu isiyopungua milioni moja. Yamkini mbegu ya haya hupandwa katika siasa za vyuo ambako mabinti huwa watazamaji wengine wanapojinoa kwa siasa za kitaifa.


No comments:

Post a Comment