ONLINE

Wednesday, 16 March 2016

NIMESADIKI HAJINYOI MWEREVU




Na Simiyu Wanyonyi        

Hii ni dhana ambayo kwa wengi huwa ni methali ya kutumia kwenye semi zao ili kuonyesha udume na udhati wao kwenye mawanda ya lugha ila kwangu sivyo. Acha hii leo tuichambue methali hii kwa kutoa maelezo yanayohusisha ukomredi wetu humu chuoni kisha tudhibitishe umuhimu wake kimaisha mbali na vitabu.

Vuta taswira ya maisha yako ukiwa Mwanafunzi wa chuo cha sekondari. Fikiria kuhusu tabia yako, ulivyokuwa ukifanya mambo yako ya kila siku chini ya sheria za shule, ukila pure iliokolea maji na chumvi na uhaba wa mafuta. Labda yalikuwa maisha mabaya au maisha mema kulingana na kuelewa kwako. Lakini angalau huko ulionekana mwerevu, mwerevu wa kufwata au kuvunja sheria hizo. Angalau kule ulijidhibiti kiusemi, kimavalio, kiafya, kiusafi na kubwa zaidi ulikuwa katibu wa saa na wakati wako wa Shughuli. Hayo angalau yalikusaidia kufuzu hadi chuo kikuu. Huko mwerevu hajinyoi ilikuwa methali ya kuimarisha stadi zako za kusema na kuandikia kupitia insha. Ilikuwa methali ya kitaaluma yaani.

Kwenye chuo, ukaja na kuwa komredi. Werevu wako ukauleta ili kuuendeleza almuradi usaidike maishani. Ukaondoka kwenye minyororo ya sheria, ukapata uhuru kutokana na werevu huo. Ukazamia nyanja uliopenda;wengine wakazamia uandishi, wengine utunzi wa nyimbo kiusanii, wengine uwanaspoti, wengine wakazama kwenye maswala ya dini na werevu zaidi wakaamua kutumia uhuru wa kujiburudisha kwa anasa za dunia.

Mwerevu hajinyoi, naam. Kwa uhodari wetu wa kusoma na kuelewa mambo kwa haraka, wengi wetu huwa wana-malevya ila wengine huelekea na kutumbukia kwenye lindi kuu ambamo kujitoa kwa hitaji uzoefu. Ulevi na matumizi ya dawa za kulevya ni la mno hapa.

Kwenye pakiti hiyo ya sigara, kuna palipoandikwa tahadhari,...'harmful to your health 'ni wazi kuwa yeyote atakayetumia dawa hii, ataadhirika kiafya. Lakini mwerevu, mwenye uwezo wa kusoma na kuelewa tahadhari hiyo hushindwa kujidhibiti na kuufukisha moshi wa sigara kama gari la kubeba taka mlimani. Anashindwa kujitahadhari.

Kwenye chupa ya pombe yoyote pia kuna ile ile tahadhari 'excessive consumption of alcohol is harmful to your health, please drink responsibly' mwenye uhuru chuoni, kwa akili na werevu wote haelewi. Ama labda huupuza tu. Shetani wa mtu ni mtu eti ila kwangu shetani ni nafsi ya mtu. Mbona tuna uwezo wa kujinyoa ila tunashindwa?

Baada ya yote, mnywaji akipata tatizo la saratani ya figo au ini, anaanza kuitisha msaada wa kuchangiwa hela ili akafanyiwe matibabu Uajemi hasa India. Mbona hukutahadhari kabla ya hatari! Baada ya kisa, mkasa. Hewala!

No comments:

Post a Comment