ONLINE

Saturday 19 March 2016

HATIMA YA CORD NA JUBILEE

Kinara wa CORD Bw. Raila Odinga ( kushoto) na Kinara wa JUBILEE Rais Uhuru Kenyatta

Na WANYONYI Simiyu

Hii ni miungano miwili kwenye siasa zozote humu nchini;ziwe za kitaifa au vyuoni. Miungano hii imejengwa kwenye misingi ya makabila ambayo kwa kiasi fulani husukumwa na ruwaza moja. Swala linalojitokeza kwa sasa ni kuwepo kwa mitazamo anwai miongoni mwa wafwasi ambao pia ni wapiga kura kwa miungano hii hasa ukizingatia siasa za humu chuoni. Je miungano hii itazidi kutamba kwenye uchaguzi wa muhula ujao au la?
Wadau wengi wa siasa humu chuoni wametabiri kuwepo kwa ushindani mkali kwenye uchaguzi unaokaribia. Wengi wanahoji kuwa huenda miungano ambayo imetawala kwa muda mrefu isiwepo tena. Wanasema iwapo itakuwepo, basi itategemea wagombea wa nyadhifa mbalimbali kutoka kwenye jamii zinazojenga miungano hiyo.
Wengi wa wapiga kura na mashabiki wametamaushwa sana na jinsi nyadhifa tofauti tofauti hugawanywa miongoni mwa jamii hizi. Mgao huo inasemekana na ni paruwanja kuwa huishia kuzua mdahalo kwani jamii moja husheheni wagombeaji wengi badala ya kuwepo kwa usawa. Kwenye mitandao ya kijamii, mikuki mingi huelekezewa jopo la wazee ama elders ambalo hujiteua huenda chemba na kuafikiana kuhusu watakao peperusha bendera ya muungano fulani. Wanasema kuwa, badala ya elders kwenda kutetea wadhifa au nyadhifa ambazo jamii imependekeza, wao huenda kule na kumtetea yeyote aliyemrambisha asali au aliyemwahidi buyu la asali iwapo angefaulu kumtetea. Ufisi huu wanalalama kuwa husababisha kufifishwa kwa ndoto ya mtu na kuiyima taasisi mwashi bora. Lakini hizi zinatosheleza kuvunjwa kwa miungano hii?
Viongozi walio kwenye nyadhifa za MUSO kwa sasa ndio kuku mgeni ambaye kwa utabiri wangu huenda akawa nuksi kwa kukuzwa kwa miungano hii kwa mara ya kwanza. Shaka Imezidi kuhusu uwajibikaji na utendakazi wa baadhi ya viongozi waliochaguliwa kwa misingi ya coalition. Kubwa zaidi ni kuwa lalama nyingi hutolewa na wale waliokaanga mbuyu huku wakihisi usaliti wa viongozi hao kwani matunda ya mti waliopanda hayaonekani. Hili laweza kuwa kama laana ambayo yesu kristo alilaani mkuyu ambao haukuwahi zaa matunda wakati huo?
Imani ya yeyote anayetambua umuhimu wa uongozi bora chuoni ni kuwa, kiongozi bora atapatikana ikiwa atapewa baraka kwa njia ya kura kutoka kwa wanazuo wa makabila, maeneo na matabaka mbalimbali kama si yote. Huyu ni kiongozi atakayechukua hatamu ya kuongoza huku dhamiri yake ikimkumbusha siku zote awajibikie kazi aliyopewa na wanazuo, bali si baadhi ya wanazuo.
Si muhali kusema kuwa kufa kwa miungano hii chuoni kutatoa nafasi kwa kiongozi mtendakazi bali si kiongozi mzembeakazini kuliongoza bewa hili aula la Moi. Hapo, tutapata mume ambaye ni moto wa koko, usipowaka utafukuta. 

No comments:

Post a Comment